
By Jamila kasimu
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa kushirikiana na Adidas limetambulisha rasmi mpira wa Kombe la Dunia 2026 unaojulikana kwa jina la TRIONDA, ambao utatumika katika michuano hiyo itakayofanyika kwa pamoja nchini Marekani, Mexico na Canada.
Jina TRIONDA limetokana na maneno ya Kihispania “Tri” linalomaanisha nchi tatu wenyeji, na “Onda” likimaanisha mawimbi. Jina hilo linaakisi ushirikiano wa kihistoria wa mataifa hayo matatu ambayo kwa mara ya kwanza yataandaa Kombe la Dunia kwa pamoja.
Mpira huo umebeba rangi za bluu, kijani na nyekundu zinazowakilisha nchi hizo tatu wenyeji. Aidha, umewekewa alama maalum zinazojumuisha jani la maple la Canada, tai wa Mexico na nyota ya Marekani.
Kwa upande wa teknolojia, TRIONDA umeboreshwa kwa kuwekwa mfumo wa kisasa wa sensa ya 500Hz ndani ya mpira, unaoweza kufuatilia kila mguso wa mchezaji na kusaidia maamuzi ya Video Assistant Referee (VAR) kwa usahihi zaidi.
Mbali na hilo, mpira huo umetengenezwa kwa muundo mpya wa paneli nne pekee, hatua inayolenga kuongeza uthabiti wa mpira pamoja na kuboresha mwendo wake hewani wakati wa mchezo.
Kombe la Dunia la FIFA 2026 linatarajiwa kuanza rasmi Juni 11, 2026, huku mechi ya ufunguzi ikipigwa katika Uwanja wa Estadio Azteca nchini Mexico. Fainali ya mashindano hayo imepangwa kuchezwa Julai 19, 2026.
